Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bi. Happiness R. Laizer leo Novemba 14, 2024 amefanya mazungumzo na Watumishi wote wa Makao makuu ya Halmashauri hiyo pamoja na Watumishi wote wa Idara ya Afya walioko Hospitali ya Wilaya ya Monduli kwa lengo la kuwakumbusha watumishi hao kufanya kazi kwa kizingatia kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa Umma.
Akizungumzia suala la kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma kwa watumishi hao wawapo kazini, Bi. Happiness amesema kuwa jambo hili ni pamoja na kuwahi kazini saa 1:30 asubuhi na kusaini kuingia na kutoka, kutekeleza wajibu mtumishi awapo kazini, suala la nidhamu na kujieshimu, mavazi kuzingatiwa.
Aidha Bi. Happiness R.Laizer amewataka watumishi hao kuzingatia utaratibu wa kujaza majukumu yao kwenye mfumo wa ess - utumishi kwani kutofanya hivyo kutapelekea kuzuiliwa mishahara pamoja na kutopata promosheni ya aina yoyote, Hivyo amewaasa wakuu wa divisheni na vitengo kuhakikisha majukumu yaliyoripotiwa na watu wa chini ya idara zao yanafanyiwa kazi na kupitishwa kwa wakati kwa ajili ya hatua nyingine.
Kwa upande mwingine Bi. Lidya Mauki Mkuu wa TAKUKURU Wilaya ya Monduli amepata fursa ya kuzungumza na watumishi hao na kuwaeleza kufanya kazi kwa uaminifu huku akisisitiza kutoshiriki vitendo vya kupokea rushwa ikiwemo zawadi zilizo kinyume na utaratibu wa maadili ya kazi.
Vilevile Bi. Lidya amewaasa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii kuzingatia Sheria na utaratibu rasmi unaofuatwa katika kukagua vikundi
vinavyostahili kupata mikopo ili vikundi vilivyotimiza vigezo pekee ndivyo vipatiwe mikopo hiyo.
Kwa upande mwingine ameitaka Divisheni ya Manunuzi kuwa wasiri na kutangaza tenda kwa kufuata utaratibu bila kuathiri maadili ya Divisheni hiyo.
Naye Bi.Rose Mhina ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Wilaya ya Monduli ameeeleza utaratibu wa vikundi vinavyochukua mikopo kwamba,kikundi kitambuliwe na afisa maendeleo ya jamii ngazi ya Kata, kipate usajili, kipate mafunzo pamoja na kukaguliwa kwa Miradi mbalimbali wanayomiliki.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli