Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Monduli Dkt. George Kasibante Leo Septemba 12, 2024 amefungua rasmi mafunzo ya siku tatu (3) yaliyo dhaminiwa na TANDIA Internation (NGO) kwa madaktari na wauguzi wa Idara ya Afya Wilayani humo, yenye dhima ya kuwawezesha watumishi hao kujikinga na magonjwa ya kuambukizwa yanayotokana na utengevu na utupaji taka za hospitalini ovyo.
Akifungua mafunzo hayo Dkt. Kasibante amewaeleza watumishi hao kuwa kupitia mafunzo haya mtaweza kukumbushwa namna bora ya kujilinda na maambukizi ya magonjwa ambayo mngeweza kuyapata kutokana na utengevu na utupaji taka mbovu katika mazingira yenu ya kazi, hii ni sambamba na kuwakumbusha suala la usafi mahali mnapofanyia kazi kwani kufanya usafi eneo lako la kazi haikuondolei cheo chako bali kukazia usafi, unadhifu na utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Aidha, Dkt. Kasibante amewaeleza watumishi hao juu ya suala la umuhimu wa utoaji huduma bora kwa Wateja na namna ya kuwajali wagonjwa wawapo vituoni kwao, " Tumeona kwamba kupitia mafunzo haya tuwakumbushe suala zima la huduma kwa wateja ili tuweze kupungua malalamiko tunayoyapata kutoka kwa Wateja wetu ambao ni wagonjwa, tutengeneze mazingira mazuri kati watoa huduma na wapokea huduma wetu ambao ni wagonjwa. " amesema Dkt. Kasibante
Ameongeza kusema kuwa tunahitaji vituo vyetu vyote viwe na mahitaji muhimu huku akiwaasa watumishi wote kuwa waaminifu Katika utendaji kazi na kwa matumizi ya rasilimali zilizopo na zinazoendelea kutolewa ili zitumike kwa matumizi sahihi yaliyokusudiwa na Serikali.
Akichangia katika ufunguzi wa mafunzo hayo Bi. Amina Bakari ambaye ni Mratibu huduma za Maabara Wilaya ya Monduli amesema "Hatutaki Mgonjwa au Mama mjamzito wakose huduma, ikiwa hakuna vifaa husika njoo utoe taarifa ili kila kituo kiwe na vifaa muhimu hasa mashine za kupima wingi wa damu tuweze kuokoa maisha ya Wananchi wetu."
Naye Dkt. Sanema Peter Mratibu wa UKIMWI Wilaya ya Monduli (DACC) Kwa niaba ya wapokea mafunzo ameeleza kufurahishwa kwake na mafunzo hayo kwani yatakuwa msaada mkubwa katika utendaji kazi wao kwakuwa lugha nzuri Kwa mgonjwa humpa matumaini ya kupona haraka na pengine kurudi tena mara anapohitaji huduma hiyo.
Dkt. Kasibante amehitimisha kwa kuwasihi watumishi hao kujitahidi Kila mmoja mahali alipo afanye kazi Kwa bidii na weledi, na ushirikiano kwakuwa sote ni Idara moja ya afya na sote tunalenga kutoa huduma bora kwa jamii.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli