Kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Monduli Ndg. Sembere Siroma ambaye pia ni Mratibu wa Uchaguzi Wilayani humo Novemba1, 2024 amezungumza na wazee wa Mila (Laigwanani) katika ukumbi wa Snake park uliopo Meserani kwa Lengo la kutoa hamasa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa malaigwani hao utakaofanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumzia Uchaguzi huo Ndg. Sembele Siroma amesema " Novemba 27, 2024 ni siku muhimu katika Taifa letu ambapo Wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la wakazi wanatakiwa kutumia siku hiyo kupiga kura ikiwa ni haki yao kisheria na kikatiba kuchagua viongozi wanaofaa watakao wasikiliza na kutatua changamoto zao ikiwemo kuwezesha kusimamia shughuli za maendeleo katika maeneo yao. Hivyo ninyi Kama Malaigwanani mnalo jukumu la kuwahamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi kama walivyojiandisha kwenda kupiga kura ili zoezi Hilo la Uchaguzi liweze kufanikiwa." Amesema Ndg. Sembere
Naye Annael Mbise kwa niaba ya Mkuu Wilaya ya Monduli amewaeleza Malaigwanani hao kuwa kufuatilia Tangazo la TAMISEMI, Novemba 27, 2024 ni siku ya mapumziko ambapo kila Mwananchi ana nafasi ya kushiriki zoezi la Uchaguzi katika eneo alilojiandikishia hivyo kwa kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ndiyo dira ya maendeleo katika nchi yetu tujitahidi tuchague viongozi wenye maono watakao wasemea katika ngazi za juu na kuwezesha kuleta maendeleo katika vijiji na vitongoji vyetu.
"Kiongozi unae mchagua ndiye atakaye leta maendeleo, kwani kiongozi unaemchagua wewe ndiye anayekusikiliza na kutatua changamoto za eneo lako." amesema Mbise
Kwa upande wake Bi.Christina Christopher Mratibu wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya ameeleza kuwa kwa kipindi hiki cha Uchaguzi tunawategemea sana Malaigwanani wetu katika maeneo mnayoishi kuhakikisha kuwa kila aliyejiandikisha kwenye daftari la wakazi katika kila kaya anajitokeza kwenda kupiga kura.
Aidha ameongeza kuwa, kwa wale vijana waliojiandikisha kabla hawajatoka kupeleka mifugo machungani wakapige kura kwanza kisha waendelee na majukumu yao ya kila siku. Hii ni sambamba na maeneo ambayo siku hiyo ni siku ya mnada viongozi (Malaigwanani) muwasisitize wananchi waanzie vituoni kupiga kura kisha wapeleke bidhaa zao Sokoni.
Vilevile, Ndg. Emmanuel Nyanda ambaye ni Afisa utamaduni Wilaya ya Monduli ametoa hamasa kwa malaigwani hao kutowaacha nyuma wanawake, vijana wa kike na wakiume waliojiandikisha katika daftari la wakazi kushiriki zoezi la kupiga kura.
Akizungumza kwa niaba ya Malaigwanani, Mzee Silonga Ngine ( Makamu Mwenyekiti wa Laigwanani Monduli) ametoa shukrani kwa Serikali kutambua uwepo wa uongozi wa wazee wa kimasai Monduli, na kuahidi kwa umoja wao kushiriki kikamilifu katika zoezi la Uchaguzi.
Akihitimisha hamasa hiyo kwa Malaigwanani, Ndg. Sembere Siroma amewasisitiza kuendelea kuhamasisha wananchi wote waliojiandikisha katika vijiji, vitongoji na kata zao kushiriki uchaguzi kwa kuchagua viongozi wenye maono ya kusimamia vema maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli