Uongozi mpya wa chama cha Mpira wa miguu (MODFA) Wilayani Monduli uliochaguliwa Machi 15, 2025 leo Machi 20, 2025 umefika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya hiyo na kukutana na Kaimu Mkurugenzi pamoja na Ofisi ya Utamaduni na Michezo, kwa lengo la kujitambulisha na kueleza malengo ya chama ili kuendelea kuboresha na kuimarisha Michezo Wilayani humo.
Akieleza malengo hayo Katika kikao kifupi kilicho jumuisha Kaimu Mkurugenzi pamoja na Kitengo cha Utamaduni na Michezo; Ndg. Yassin Hamis Hassan katibu wa chama hicho ameeleza kuwa MODFA inalenga kuibua vipaji mbalimbali hasa mashuleni kuanzia ngazi ya msingi, kuvikuza na kuviendeleza ili kuhakikisha kunakuwepo na wanasoka wengi nchini wanaotokea Wilaya ya Monduli.
" Tunatarajia kufanya bonanza kubwa linalolenga kutambulisha viongozi wapya katika Kata ya Mto wa Mbu, bonanza litakaloweka alama ya kuanza kufanya kazi kwa Kasi na weledi ambapo tiyari amepatikana mfadhili atakayewezesha bonanza hilo na yuko tayari kuweka taa katika eneo la kiwanja hicho cha Mto wa Mbu." amesema Ndg. Yassin
Kwa upande wake Ndg. Abubakari Hamis Mwenyekiti wa MODFA ameomba Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli kutenga eneo maalum la uwanja wa Michezo wa Wilaya huku akiomba ushirikiano na kwamba MODFA iko tayari kushauriwa ili kuleta ufanisi mkubwa katika Michezo Wilayani humo.
Naye Ndg. Richard Ngoda Afisa Michezo Halmashauri ya Wilaya ya Monduli amewapongeza viongozi wapya na kusema ". Tunayo Imani kubwa na ninyi mliopata uongozi na tunataraji kuona wachezaji wengi wa Monduli wanashiriki ligi kuu , pia klabu za Monduli MBUNI na TMA zinapanda ligi kuu." amesema Ndg. Ngoda
Vilevile Ndg. Emmanuel Nyanda Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni na Michezo amewataka viongozi hao kuzingatia uwekaji taarifa katika maandishi kwa ajili ya rejea ,ushirikiano huku akisisitiza kuepuka migogoro ambayo inaweza kuleta mpasuko ndani ya chama na kuzorotesha Michezo Monduli.
Akihitimisha kikao hicho Bi. Pamela Ijumba Kaimu Mkurugenzi amesema suala la kiwanja cha Michezo litafanyiwa kazi na uongozi wa Halmashauri na pia viwanja vilivyopo washirikisheni wadau viboreshwe ili viweze kutumika.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli