Idara ya kilimo, mifugo, na uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli yaaswa pamoja na kuelimisha kilimo cha mazao mbali mbali, ihamasishe zaidi kilimo cha mazao jamii ya mikunde, yakiwemo maharage hasa katika msimu huu wa mvua za vuli ili kuwepo kwa utosherevu wa mazao hayo ambapo sasa bei yake imepanda kutokana na uhitaji mkubwa kwa jamii hasa mashuleni.
Hayo yamesemwa Novemba 1, 2024 na Bi. Rose Mhina kwa niaba ya Bi. Happiness R. Laizer Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, katika kikao cha Kamati Mseto ya Lishe yenye lengo la kujadili shughuli za Lishe zilizotekelezwa na idara mtambuka kwa kipindi cha robo ya kwanza Julai hadi Septemba kwa mwaka wa fedha 2024/2025 katika ukumbi wa udhibiti Ubora wa Elimu Wilayani hapo.
Akiwasilisha Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Lishe katika idara ya Afya Ndg. Michael Mhombo ambaye ni Afisa Lishe wa Wilaya ya Monduli ameeleza kuwa Wilaya hiyo Ina jumla ya watoto elfu 42.9 chini ya miaka mitano (5) kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2022, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Halmashauri imetenga shilingi million 66.3 kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Lishe Wilayani humo.
Akifafanua shughuli hizo Ndg. Michael ametaja shughuli tisa (9) zilizofanyika katika robo ya kwanza ikiwemo maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji pamoja na uboreshaji wa huduma za Lishe katika wodi ya watoto hospitali ya Wilaya ya Monduli.
Kufuatia uboreshaji huduma hiyo jumla ya watoto elfu 25.5 walipimwa, na watoto 2 pekee waligundulika na changamoto ya utapia mlo mkali huku watoto 94 wakiwa na utapia mlo wa kadri, ambapo wamepatiwa huduma na afya zao zimeimarika.
Aidha, Bi. Magreth Muro Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Monduli ameeleza hali ya Lishe kwa wanafunzi kuwa ni nzuri huku akisisitiza uwepo wa mlo kamili kwa wanafunzi hao kwa kuzingatia ratiba zao za chakula pamoja na mbogamboga na matunda, ukizingatia Wilaya ya Monduli ni moja ya Wilaya ambayo Shule zote za Sekondari za Serikali ni za Bweni.
Kwa upande wake Bi. Adventina Nyambuya ameshauri kuwepo kwa hamasa kubwa za Lishe mashuleni kupitia Club za Lishe
Zilizopo mashuleni, wanafunzi wahimizwe kuweka bustani za mboga mboga na kupanda mti wa matunda na kuutunza ili kuwepo matunda ya kutosha kwa ajili ya kubotesha afya zao wawapo shuleni.
Bi. Rose Mhina amehitimisha kikao hicho kwa kuwataka wajumbe hao kuendelea kutoa elimu ya Lishe bora kwa Jamii ikiwa ni pamoja na kuifanya ajenda ya usafi na kunawa mikono kuwa ajenda ya kudumu nyumbani, kazini na mashuleni ili kuepuka ama kuondoa kabisa magonjwa ya tumbo na ya mlipuko yatokanayo na uchafu kwakuwa huwezi kutenganisha Lishe bora na usafi.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli