he. Isaack Copriano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ameongoza kikao cha Baraza la Madiwani la robo ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Novemba 6, 2024 katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri hiyo, chenye dhima ya kujadili Utekelezaji wa taarifa kutoka Kamati mbalimbali ikiwemo Kamati ya Masuala ya Maji Wilayani hapo.
Akizungumzia suala la Uhaba wa Maji kwa wananchi na mifugo katika Baraza hilo Mhe. Isaack Copriano amesema " suala la Uhaba wa Maji limekuwa ni changamoto kubwa sana ndani ya Wilaya ya Monduli hasa katika kipindi hiki cha msimu wa kiangazi jambo linalopelekea sasa akina Mama kutumia muda mrefu kwenda umbali mrefu zaidi kutafuta Maji bila mafanikio huku mifugo ikidhurika kwa kukosa Maji." amesema Ndg. Isaack Copriano
Akichangia mada katika Kamati hiyo kuhusu Maji Mhe. Thomas Meyan Diwani wa Kata ya Monduli juu, ameshauri kwamba kama Kuna mchakato wowote wa mradi wa Maji unaoendelea uwekwe msukumo wa kukamilisha mradi wa Maji ulioko Monduli juu ambao haukukamilika ili Maji hayo yawanufaishe wananchi wote.
Naye Ndg. Naville Daud Msaki Meneja wa RUWASA Wilaya ya Monduli ametoa ufafanuzi wa suala la Uhaba wa Maji na kusema " Ni kweli changamoto hiyo ipo na Sisi kama RUWASA tumechukua hatua kwa kuandika barua kwa Waziri wa Maji kueleza changamoto hii ikiwa ni pamoja na kuainisha katika bajeti tuliyoweka jumla ya vijiji ambavyo havina huduma rasmi ya Maji huku tukionyesha mchanganuo wa njia mbadala ya kupata Maji katika maeneo hayo kwa kutumia gari la mamlaka ya Maji ambapo kwa mwezi itagharimu shilingi milioni 255 na kwa kukodi gari binafsi ni milioni 390." amesema Ndg. Msaki
Kwa upande mwingine CPA. Ramadan S. Madeleka ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Usimamizi, ufuatiliaji na Ukaguzi ameshauri juu ya namna nzuri ya uendeshaji wa Baraza huku akisisitiza taarifa kupitia kwenye Kamati husika na kuhakikiwa kabla na si kuletwa wakati wa Baraza.
Ameongeza kusema kuwa, licha ya kuipongeza Monduli kwa ukusanyaji wa mapato pia kwa mwaka huu nawapongeza kwa Usimamizi mzuri wa miradi ukilinganisha na wakati ulopita huku akiwataka kutumia fedha zilizoletwa na Serikali kwa ajili ya miradi kwa wakati na si kuziacha kwenye akaunti.
Sambamba na hayo CPA. Ramadan S. Madeleka ameshauri Halmashauri hiyo kuweka mkakati wa ulipaji madeni ya watumishi na wazabuni huku akielekeza namna nzuri ya kupunguza hoja kwa Halmashauri hiyo.
Bi. Happiness R. Laizer Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ameahidi kuendelea kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato huku akieleza changamoto ya mafundi kuomba tenda za ujenzi kupitia mfumo kuwa jambo linalochelewesha ukamilishwaji wa miradi kwa wakati.
Akihitimisha kikao hicho cha Baraza Ndg. Isaack Copriano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Monduli amewaomba AUWSA na RUWASA Kusaidia kutoa gari ili yawekwe mafuta kwa ajili ya kupeleka Maji mashuleni ambako pia hali ya upatikanaji wa Maji ni ngumu. Pia ameomba baadhi ya maeneo yenye changamoto kubwa ya Maji yaongezewe idadi ya siku za kupata maji kwa mgao wa maji uliopo.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli