Jamii ya Kimasai, imefika hatua sasa tuachane na tabia ya kufunga peke yake badala yake tujikite pia katika kilimo hasa kilimo cha mazao ya biashara ambayo yatatuvusha na kutupandisha kiuchumi.
Hayo yamesemwa Desemba 14, 2024 na Mhe. Festo Shem Kiswaga Mkuu wa Wilaya ya Monduli alipokuwa akizungumza na Wananchi wa Kata ya Monduli Juu, katika tukio la kueleza malengo ya msimu wa kilimo kwa awamu ya kwanza kwa ukanda wa Halmashauri hiyo.
Mhe. Kiswaga ametoa jumla ya kilo 400 za mbegu za choroko, mbaazi na alizeti kwa wakulima wa Kata ya Monduli Juu huku akieleza kuwa katika msimu huu wa kilimo analenga kila Mwananchi wa Monduli lazima alime jumla ya ekari 4 ambapo ekari 2 zipandwe choroko na ekari 2 zipandwe mbaazi bila kusahau zao la alizeti; kwani hii itatusaidia kujikwamua kiuchumi. amesema Mhe. Kiswaga
Naye Bi. Pamela Ijumba ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Kilimo Wilaya Monduli amezungumza na wakulima hao wa Monduli Juu huku akiwasisitiza kuzingatia kilimo bora cha kisasa kwa kupima Afya ya udongo wa mashamba yao kabla ya kupanda mbegu, ambapo amesema huduma hiyo hutolewa bure.
Bi. Pamela ameongoza kusema kuwa, wakulima hao wanapaswa kuzingatia matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo ikiwemo kuchagua mbegu bora zinazostahimili hali ya ukanda husika ili kupata uzalishaji bora na wenye tija.
Aidha, Bi. Pamela amewaomba Wadau mbalimbali kushirikiana na wakulima hao ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija na kufikia malengo ya AGENDA 10/30.
Kwa upande wake Mhe. Thomas Meyan Diwani wa Kata ya Monduli Juu, ameeleza uhitaji wa wakulima wa Kata hiyo na kusema " Tunahitaji tupate duka la pembejeo za kilimo katika Kata yetu kwa kuwa tuna soko hapa ambapo wakulima wanauzia mazao yao ambayo hipimwa kwa madebe yasiyo na kipimo Maalum lakini pia wakulima hawa wapatiwe mizani ya kupimia mazao yao ili waweze kuuza kwa faida.
Vilevile Mhe. Meyani ameiomba Divisheni ya Kilimo Wilayani hapo kuhakikisha wanawafundisha wakulima kuweka Kingamaji kwenye mashamba ili kuzuia mmomonyoko unaopelekea kupunguza rutuba katika mashamba hayo.
Kwa upande mwingine Ndg. Edward Ngobei Mmoja wa Wakulima katika Kata hiyo, ameshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuboresha huduma za ugani ambapo sasa Mkulima anajipatia ushauri, bei na mabadiliko yake kupitia mfumo; lakini pia katoa shukrani kwa kupatiwa mbegu hizo na kuahidi kufanya kazi kwa bidii.
Mhe. Kiswaga amehitimisha kwa kutoa agizo kuwa trekta mbili zilizopo Monduli wakati wa msimu wa masika zitumike kuwasaidia Wakulima wa shairi kwa gharama ya shilingi elfu arobaini na tano tu (45,000) kwa ekari moja.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli