Bi. Pamela Ijumba Mkuu wa Divisheni ya Kilimo na Mifugo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bi. Happiness R. Laizer leo Desemba 17, 2024 katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo, amefungua kikao kazi cha kujadili mpango wa awali wa bajeti ya Lishe kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akizungumza katika kikao hicho Bi. Pamela amesema " Lishe bora ni suala muhimu sana katika jamii na uzingatiaji wake unatusaidia kuondokana na Masuala ya udumavu kwa Watoto pia kuwa na kizazi chenye Afya na akili njema. " amesema Bi. Pamela
Aidha, Bi. Pamela ameitaka Idara ya Afya na Elimu kuendelea kutoa elimu ya Lishe kwa jamii na kwa Wanafunzi pia huku akisisitiza utoaji wa vitamini 'A' na virutubisho kwa Watoto wachanga ikiwemo kuzingatia ulaji wa Lishe bora kwa Wanafunzi wawapo mashuleni.
Akitoa wasilisho la hali ya Lishe la Mkoa wa Arusha Bi. Dotto Milembe, Afisa Lishe kutoka Mkoani amesema kuwa bado iko sababu ya kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii kwani changamoto ya anemia kwa mama wajawazito na uzito mdogo kwa Watoto kutokana na Lishe mbavu Wilayani Monduli bado ipo kwa takeimu za 272 Wanawake na 15758 kwa Watoto.
Bi. Dotto ameshauri Wanawake wenye changamoto ya anemia wapewe vidonge vya kuongeza damu ili kupunguza tatizo la vifo vya akina Mama hao wakati wa kujifungua huku akishauri uzalishaji wa vyakula bora, uwepo wa bustani za mboga mboga mashuleni pamoja na uanzishwaji wa klabu za Lishe mashuleni ili elimu ya ulaji sahihi wa vyakula vyenye virutubisho ienee kuanzia shuleni hadi kwa Jamii yote.
Kwa upande wake Dkt. Kasibante Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Monduli amesisitiza kuwa Mpango wa awali wa bajeti uliojadiliwa, baada ya maboresho kwa maeneo yaliyopendekezwa na wajumbe, yazingatiwe ili bajeti mpya ijayo maeneo hayo yapewe kipaumbele ili Wilaya ya Monduli iweze kufikia malengo katika Masuala ya Lishe bora.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli