Mkuu wa wilaya ya Monduli Mhe. Idd Hassan Kimanta amekabidhi hati za malipo zenye thamani ya jumla ya Tsh millioni 115 kwa vikundi 26 vya wanawake na vijana wilayani Monduli . Fedha hizo zinazotokana na asilimia 10 ya makusanya ya ndani ya Halmashauri. Tukio hili lilifanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Monduli tarehe 12 Julai 2018.
Akizungumza katika hafla hii, Mhe. Kimanta alinza kwa kuwapongeza wale wote wanaorudisha mikopo kwa uaminifu. Aliwaelekeza maafisa maendeleo ya kata kuwa ni wajibu wao kuhamasisha na kuunda vikundi vya ujasiriamali ili wananchi watumie fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri. Hali kadhalika amevitaka vikundi vinavyonufaika na mikopo hii kuwa na ubunifu kwa kutumia soko lililopo Wilayani Monduli, akitoa mfano wa kushona na kuuza sare za shule, soko la nyama za kuku katika ‘camp sites’ zilizopo eneo la Mto Wa Mbu na kuanzisha vikundi vya utengenezaji na usambazaji wa mikate Monduli Mjini.
Hafla hii ilihudhuriwa pia na Mhe. Julius Kalanga(Mbunge) na Mhe. Isaac Joseph (Mwenyekiti wa Halmashauri).
Mhe. Mwnyekiti wa Halmashauri naye aliposimama, alianza kwa kuwapongeza akina mama kwa kuhamasika kuuunda vikundi kwa ajili ya kutumia fursa hii ya mikopo. Alisema akina mama wanaaminika na mara nyingi wamekuwa waaminifu kurudisha mikopo wanayopewa kwa muda unaohitajika. Mhe. Isaac aliwatahadharisha wahusika kuwa wanapochukua mikopo wafanye biashara wenyewe wasimpatie mtu mwingine kufanyia biashara au kufanyika kwa matumizi mengine.
Kabla ya kumkaribisha Mkuu wa wilaya; Mhe. Mbuge wa Monduli alianza kwa kusisitiza kuwa katika tukio kubwa la namna ile madiwani wote wangepaswa kuwepo ili kushuhudia matunda ya kazi yao. Pia akapendekeza kuandaliwa kwa kongamano la elimu ya ujasiriamali kwa vijana ili vijana nao wanufaike na mikopo hii kama ilivyo kwa akina mama.
Hali kadhalika Rose Mhina ambaye ni Mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii katika Halmashauri ya wilaya ya monduli akiongea kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji (W) alisema, changamoto kubwa Halmashauri inayokabiliana nayo ni; baadhi ya vikundi kutokuwa waaminifu kwa kubadili madhumuni ya mikopo waliyoomba na kufanya shughuli nyingine na kusababisha vikundu hivi kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.
Vikundi vilivyopatiwa mikopo vinatoka kata za Engaruka, majengo, Monduli mjini, Lemooti, Engutoto, Migungani, Mto wa mbu, Moita, Meserani, Makuyuni, Lolksale na Selela. Kuna jumla ya vikudi 26 vyenye jumla ya wanachama 531.
Imeandikwa na;
E.Msifuni,
Afisa TEHAMA (W)
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli