Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa Jumla ya Shilingi Bilioni 14.4 kwaajili ya fidia kwa Wakazi wa Vijiji vinne vilivyopo kwenye Kata ya Engaruka Wilayani Monduli Mkoani Arusha ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya sita katika uendelezaji na Utekelezaji wa miradi ya Kimkakati yenye tija kwa Taifa.
Akizungumza kwaniaba ya Rais Samia Suluhu Hassan Januari 23, 2025. Mhe. Dkt. Selemani Jafo Waziri wa Viwanda na biashara wakati akizindua ugawaji wa fidia hizo kwa awamu ya kwanza yenye takribani Bilioni 6.2 amewataka wasimamizi wa zoezi hilo kuhakikisha kuwa ulipaji wa fidia hizo unakamilika kabla ya Februari 15, 2025 huku akiagiza shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kushughulikia malalamiko yote ya fidia kwa wananchi wa eneo hilo ili kila mwenye haki ya kufidiwa apate haki yake.
Kwa upande wake Mhe. Jofrey Pinda Naibu Waziri wa Ardhi amesema " Serikali imeweka mpango maalum wa kuhakikisha kuwa eneo la Engaruka linakuwa na barabara zinazopitika muda wote, maji pamoja na upatikanaji wa umeme mkubwa wa Kilowati 33 ili kusaidia katika shughuli za uendeshaji wa viwanda viwili vikubwa vinavyotarajiwa kutekeleza mradi huo." amesema Mhe. Pinda
Naye Mhe. Paul Makonda Mkuu wa Mkoa wa Arusha amesema kuwa, Arusha ni miongoni mwa mikoa yenye bahati na kadri siku zinavyosonga, Mkoa huu utatoa fursa mbalimbali za maendeleo kwenye sekta za Kilimo, Madini na Michezo, zitakazosaidia wananchi kujikwamua kiuchumi hivyo kupitia mradi huu wa magadisoda kipaumbele cha ajira kitolewe kwa wazawa wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Arusha.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa Kimkakati, Mkurugenzi mwendeshaji wa NDC Dkt.Nicolaus Shombe amesema mradi huo wa magadi soda umechukua zaidi ya miaka 29 tangu mchakato wake ulipoanza baada ya NDC kufanya utafiti wake na kubaini uwepo wa magadisoda yenye kufikia mita za ujazo Bilioni 3.8 sawa na tani Milioni 787 ambapo kupitia utekelezaji wake, viwanda viwili vikubwa vitakavyogharimu Trilioni 1.6 vitajengwa katika eneo hilo lenye jumla ya ekari elfu 60, 884.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli