Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Said Jafo, January 10, 2025 amezungumza na Wananchi wa Engaruka katika zoezi la uhamasishaji kuelekea ulipaji wa fidia kwa wakazi wa maeneo hayo ambapo Serikali inatarajia kulipa kiasi cha shilingi bilioni 14.4 kwa wananchi wanaotakiwa kupisha utekelezaji wa mradi wa maendeleo wa uchimbaji wa madini ya magadi soda katika Kata ya Engaruka, iliopo Wilayani Monduli.
Akieleza zaidi, Dkt. Jafo amesisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha fidia inalipwa kwa uwazi, haki, na kwa kuzingatia thamani halisi ya mali za kila mwananchi anayeguswa na mradi huo.
Katika mkutano huo, Waziri Jafo alibainisha mambo muhimu yanayozingatiwa katika ulipaji fidia hiyo kuwa ni
Wafidiwa Watalipwa Kwa Haki na Uwiano; Waziri alisisitiza kuwa Serikali imehakikisha kuwa jumla ya wafidiwa 595 watalipwa fidia kwa kiwango kinacholingana na tathmini iliyofanyika huku akiweka bayana kuwa hakuna mwananchi atakayedhulumiwa au kupunjwa malipo.
Pia, Ili kuhakikisha matumizi bora ya fedha za fidia, Serikali kwa kushirikiana na NDC na taasisi nyingine za kifedha kama UTT-AMIS, NEEC, NMB, na CRDB, imeandaa semina za kuwaelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha hizo.
Ameongeza kusema kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ya Magadi Soda unatarajiwa kuanza mara baada ya ulipaji fidia, na kwamba mradi huo utatoa ajira kwa wananchi wa eneo husika na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla huku akiwataka wananchi wa Kata ya Engaruka kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa bila changamoto.
“Serikali iko nanyi, na dhamira yetu ni kuona kila mmoja wenu anapata haki yake. Tushirikiane kuhakikisha mafanikio ya pamoja yanapatikana. " Amesema Dr. Jafo
Awali, akizungumza wakati wa mkutano huu wa hadhara, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC. Dkt. Nicolaus Shombe amebainisha kuwa tayari NDC imejipanga vizuri kuelekea utekelezaji wa zoezi hilo ambalo linatarajia kuzinduliwa rasmi mwezi Januari, 2025.
Ndg. Pele Saningo mmoja kati ya jumla ya wanufaika 595 ameshukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuona umuhimu na kuwajali.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli