Leo *alhamis* tarehe 12 Aprili 2018, EDWARD MORINGE SOKOINE, kipenzi cha watanzania, ametimiza miaka 34 toka afariki.
SOKOINE alikuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kwa vipindi viwili ambapo mara ya kwanza aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Rais JULIUS KAMBARAGE NYERERE tarehe 13 Februari 1977.
Tarehe 7 Novemba 1980, SOKOINE alijiuzuru na kwenda kusoma Yugoslavia na aliporudi, aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu tarehe 24 Novemba 1983. Alishikilia wadhifa huo hadi tarehe 12 Aprili 1984 alipopata ajali ya gari na kufariki dunia. Benzi lake liligongwa na Toyota Land Cruizer lililokuwa likiendeshwa na DUMISAN DUBE, raia wa Afrika Kusini, eneo la Dakawa, kilomita 40 toka Morogoro. SOKOINE alikuwa akitokea bungeni Dodoma na kauli yake ya mwisho bungeni alisema:*"Tutakutana tena kwa kikao kijacho cha bunge hapa Dodoma. Safari hii sitaki kurudi Dar es Salaam kwa ndege, nitasafiri kwa gari nijionee hali ya mazao ya wakukima"*.
SOKOINE alikaa kiti cha nyuma na hakufunga mkanda. Hivyo, ajali ilipotokea alirushwa hadi kioo cha mbele na kuumia sana kifuani na shingoni. Alipofikiswa hospitali ya mkoa wa Morogoro, madaktari walithibitisha amefariki.
Majira ya saa 10 jioni siku hiyo ya *alhamis* tarehe 12 Aprili 1984 huku mvua za manyunyu zikirindima jijini Dar Es Salaam, ghafla vipindi vya RTD vilikatizwa na ukapigwa wimbo wa Taifa. Mara Rais NYERERE, kwa huzuni kubwa, akalitangazia taifa kama ifuatavyo:*Ndugu wananchi, leo saa 7 mchana ndugu yetu, kijana wetu EDWARD MORINGE SOKOINE ambaye alikuwa akisafiri kwa gari toka Dodoma amepata ajali na amefariki..Ndugu wananchi nawaombeni muamini EDWARD amefariki kwa ajali ya gari......"*.
NYERERE alipomaliza tu kutangaza habari hiyo, ilikuwa ni vilio na simanzi nchi nzima. Mwili uliwasili Ikulu saa 11 ukiwa umefunikwa kwa bendera ya Taifa na mlinzi wake akaufunua. NYERERE akiongozana na Mama MARIA, alimshika usoni SOKOINE kwa huzuni kubwa kisha akaiweka mikono yake miwili kwenye paji la uso wake na kulia kwa huzuni hadi akaondolewa na walinzi wake.
Mwili ulipelekwa hospitali ya Lugalo na kesho yake Ijumaa ulipelekwa Karimjee Hall ambako maelfu ya watanzania walienda kumuaga kipenzi chao.
Jumamosi, mwili ulipelekwa airport ambapo Daladala zote jijini ziliwapeleka na kuwarudisha wananchi bure bila kulipa nauli. Hii ilikuwa ni shukrani yao kwake kwani SOKOINE ndiye alikuwa mwasisi wa Daladala. Mwaka 1983, baada ya kuona UDA imezidiwa, ndipo alipoanzisha utaratibu wa Daladala.
Mwili ukasafirishwa kwenda kwao Monduli Juu. Jenerali JOHN BUTLER WARDEN, Mtanzania chotara, ndiye aliyejenga kaburi la SOKOINE la aina yake akisaidiwa na askari wa TPDF. Jenerali WARDEN ndiye pia aliyejenga kaburi la Rais SAMORA MOISES MACHEL mwaka 1986. SOKOINE akazikwa kwa huzuni kubwa mno.
SOKOINE alililiwa na maelfu ya watanzania nchi nzima. Msiba wake ulikuwa mkubwa kuliko yote iliyowahikutoka nchini, rekodi ambayo ilikuja kuvunjwa na msiba wa Baba wa Taifa mwaka 1999.
SOKOINE aliacha wajane 2 na watoto 11.
SOKOINE alikuwa ni kiongozi wa kipekee. Ukimuondoa Baba wa Taifa, Tanzania haijawahi kuwa na kiongozi *Mzalendo wa kweli* kama yeye.
SOKOINE alikuwa kiongozi shupavu, mkweli, mwema mwenye sauti ya upole, mpenda watu, mchukia rushwa na wabadhilifu wa mali ya umma.
Daima SOKOINE, tofauti na viongozi wengi wa Afrika, aliishi alivyohubiri. Hakutumia cheo chake kujinufaisha yeye binafsi wala watu wa kwao Monduli. Kwake yeye, watu wa maeneo yote nchini walikuwa ni wananchi wake na aliwahudumia bila kuwapendelea wala kuwabagua.
SOKOINE hakuwa mwenye tamaa ya mali kama walivyo viongozi wengi wa miaka hii, bali aliishi maisha kama ya mtanzania wa kawaida. SOKOINE alianzisha *Presidential Trust Fund* Ikulu na akawa anaweka mshahara wake ili kuwasaidia wakina mama kuweza kukopa. Kwa hakika, alikuwa kiongozi wa kipekee.
SOKOINE alikuwa mchapakazi hodari na mbunifu. Aliwachukia sana wazembe. Alikuwa akifanya kazi mchana na mara nyingi hadi usiku na alikuwa mfuatiliaji mkubwa wa utekelezaji wa maagizo yake. Tanzania haijawahi kupata kiongozi mwenye kumbukumbu (photographic memory) kama SOKOINE. Aliwaumbua wote waliosahau, kuchelewesha au kushindwa utekelezaji wa maagizo yake.
SOKOINE aliwachagua vijana wawili hodari na wachapakazi (Bw. PHILEMON LUHANJO na MARTENS LUMBANGA) ambao walikuwa chini ya Katibu HORRACE KOLIMBA. Hawa watatu walibatizwa jina la utani *"Wafuasi wa SOKOINE"* na walifuatana nae sehemu mbalimbali nchini. Vijana hawa wa enzi hizo, walimsaidia sana SOKOINE.
Nukuu zifuatazo zitasaidia kuwapa mwanga wale ambao hawakumjua, ili kujua SOKOINE alikuwa ni mtu wa aina gani:
1. *"Ole wake kiongozi mzembe na asie na nidhamu nitakaemkuta. Kiongozi wa siasa hana usalama wowote. Usalama wake ni kudra ya Mungu na wananchi tu. Viongozi wazembe na wabadhilifu wahesabu siku zao, labda tusiwajue."*26 Machi 1983.
2. *"Wajibu wa kila mtanzania, kila familia na kila anaekula ni kujilisha mwenyewe. Sio wajibu wa serikali kumlisha mtu. Unaweza ukasaidiwa unapopatikana na janga. Lakini kama hakuna janga ni wajibu wa kila mtu kujitosheleza na kutoa faida kwa Taifa"*.4 Octoba 1983
3. *"Vijana wengi leo wana mali sana kuliko wazee wao waliofanyakazi serikalini kwa miaka 30 hadi 40. Lakini wazee wanaitaka serikali ndiyo iwaulize vijana hao mali hizo wamezipata wapi. Hivi kwanini mzazi usimuulize mwanao-"mali hizi umezipata wapi?"*.23 Octoba 1983.
4. *"Suala la uzalendo lazma tulifikirie tunapotaka kuchagua viongozi wa kitaifa. Naskia huko mikoani kuna baadhi ya viongozi wanagombea nyumba na magari. Mambo haya si ya muhimu. Viongozi watafanya vizuri wakigombea maendeleo ya wanavijiji. Huo utakuwa ugomvi mtakatifu"*.11 Machi 1982
5. *"Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi kuwa chombo cha kulinda haki na maslahi ya wengi. Na kamwe hayaruhusiwi kuwa chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao na kusahau maslahi ya wengi"*.1 Februari 1977
Rais wetu mpendwa wa Jamhuri ya Tanzania Mh. DR. JOHN JOSEPH POMBE MAGUFULI nae amemuelezea SOKOINE alivyomfahamu:
*"SOKOINE alikuwa kiongozi shupavu aliyewapenda watanzania na kuchukia ufisadi. Namuona ni kielelezo cha pekee Tanzania. Tarehe 12 April 1984, mimi nilikuwa JKT Mpwapwa, ilikuwa siku ya majonzi makubwa"*.Rais JPM, 12 April 2016.
*Je, watanzania tunamuenzi vipi shujaa huyu?*
*USHAURI*:
1. Viongozi wa serikali acheni utamaduni wa kuwaenzi viongozi hawa akiwemo SOKOINE kwa maneno tu, bali muwaenzi kwa vitendo.
2. Wapinzani acheni kuamini kuwa jukumu la kumuenzi SOKOINE ni la serikali tu. Hata nyie mnnapaswa kumuenzi kivitendo.
3. Kila mtanzania unapaswa kumuenzi SOKOINE kwa kutenda yote mazuri aliyohimiza.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli