Ninawataka Maafisa Elimu Kata, Watendaji wa Kata, Maafisa Tarafa kwa pamoja kuwahamasisha na kuwafahamisha Wananchi wote katika maeneo yenu, ili wajue fursa hizi za Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi; mkibainisha umuhimu na manufaa yake kwa Jamii ili kusaidia jamii kuondokana na dhana potofu iliyojengeka kwa wananchi juu ya elimu hii na kuwafanya wengi wenye uwezo kutojiunga nayo.
Hayo yamesemwa leo Septemba 13, 2025 na Mhe. Gloriana Julius Kimath Mkuu wa Wilaya ya Monduli katika Siku ya Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi yaliyofanyika katika viwanja vya Polisi Mjini Monduli.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo Mhe. Gloriana amewashukuru wadau wote wa elimu ya watu Wazima na Elimu nje ya mfumo rasmi akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli na wadau wote waliochangia kufanikisha maadhimisho hayo.
Akisoma taarifa ya Maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bi. Happiness R. Laizer, Mwl. Magreth Muro ambaye pia ni Kaimu Afisa Elimu Sekondari katika Halmashauri hiyo amesema kuwa; awali Wanakisomo hao walijifunza kusoma, kuandika na kuhesabu tu maarufu kama GUMBARU lakini sasa Wanakisomo hao hujifunza na kuunda vikundi tofauti tofauti vya uzalishaji Mali na wengine hupata fursa za kujiendeleza na Elimu ya juu ambapo kwa Monduli Kuna jumla ya vituo 33 yaani 27 vya MEMKWA na 6 vya MUKEJA. kwa mwaka huu wa 2025 Wilaya ya Monduli jumla ya Wanakisomo 551 wamejiunga na Programu ya MEMKWA ambayo hujumuisha makundi rika mawili kuanzia umri wa miaka 9 hadi 13 na kundi la miaka 14 hadi 17; huku kupitia MUKEJA inayo husisha miaka 18 na kuendelea wakijiunga watu 1,050.
Ambapo, Wanakisomo hao hujifunza ujasiriamali, ushonaji, useremala, umeme wa majumbani, upishi, upambaji, uongozaji wa Watalii pamoja na kujifunza stadium za kusoma, kuandika, na kuhesabu kwa wasio na stadi hizo.
Mwl. Magreth Muro licha ya kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa kutokana na utekelezaji wa programu hizo, ameeleza pia changamoto zinazokabili utoaji wa elimu kwa Wanakisomo hao kuwa ni pamoja na dhana potofu ya Jamii kuhusu Elimu husika, wahitaji wa elimu hiyo kuogopa kuchekwa, kuwepo wa vituo vichache, upungufu wa walimu wa ufundi na vifaa.
Kwa upande wake Bi. Suzan Mollel mmoja wa wanufaika wa elimu hiyo Wilayani Monduli, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kusimamia utoaji wa elimu hii na kuomba Jamii kuwa na mtazamo chanya juu ya elimu hii kwani imesaidia katika kuimarisha uchumi wa wengi kwa Maendeleo ya Jamii na Taifa pia.
Kaulimbiu: " Kuza kisomo katika zama za kidigitali kwa maendeleo endelevu ya Taifa letu. "
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli