Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Kenani Laban Kihongosi leo Agosti 08, 2025 wakati akizungumza na Maelfu ya wananchi waliohudhuria Sikukuu ya Wakulima nchini maarufu kama Nanenane, ametoa wito kwa wananchi kusimama imara katika kulinda na kutunza amani ya Mikoa ya Kanda ya Kaskazini na Tanzania kwa Ujumla, akiwataka kujiepusha na wanaohamasisha vurugu kwani amani iliyopo nchini ndiyo msingi wa maendeleo makubwa yanayoshuhudiwa chini ya serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Ndugu wananchi tusikubali kwa namna yoyote tukashawishiwa na kwenda kufanya vitendo visivyofaa ndani ya Mikoa yetu. Lindeni uhai wenu, lindeni amani yenu, lindeni taifa lenu, tukiharibu nchi hii hatuna nchi nyingine." Amebainisha Mhe. Kihongosi.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa Mkoani Arusha ndani ya Miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia kwenye Sekta ya Kilimo, afya, Miundombinu, elimu, viwanda na biashara, Mhe. Kihongosi amesisitiza pia umuhimu wa wananchi kushiriki kwenye Uchaguzi Mkuu kwa kuchagua Viongozi waadilifu na wachapakazi kwa maendeleo ya sekta ya Kilimo, uvuvi na ufugaji.
Aidha kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu, akirejea hotuba ya Mhe. Kihongosi amemtaja Rais Samia kama Kiongozi aliyefanikisha miradi mingi ya Maendeleo kwenye Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, akiwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Rais Samia kutokana na miradi mingi aliyoitekeleza kwenye Kanda hii.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Nanenane kwa mwaka 2025 yaliyofanyika Kikanda kwenye Viwanja vya Themi- Njiro Mkoani Arusha inasema "Chagua Viongozi bora kwa maendeleo endelevu ya kilimo, mifugo na uvuvi 2025."
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli