Wilaya ya Monduli Mkoani Arusha - Tanzania, ni miongoni mwa Wilaya zilizobahatika kutembelewa na Wataalam kutoka Helenkeller International (HKI), ambao wameweza kuanzisha program za SWASH na F and E mashuleni (behavior change)kwa kutoa Elimu kwa walimu 93 wa shule 93 za Msingi ambao wameanzisha klabu za SWASH na Michezo ya karata zenye jumbe za kuwawezesha Wanafunzi hao kuwafundisha wenzao na Wazazi huku wakiimarisha usafi wa Mazingira kwa Lengo la kutokomeza Trakoma katika Jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Happiness R. Laizer, Ndg. Haruna Haji (wa pili kulia) ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Biashara Viwanda na Uwekezaji amewakaribisha wageni hao kwa kusema anatambua mchango wao kwa Jamii ya Monduli na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano huku akitoa wito kwa wageni hao kuleta program nyingine kwakuwa nahitaji ni makubwa.
Naye Dkt. George Kasibante (wa pili kushoto) Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ameueleza ugeni huo kuwa " Tunahudumia Jamii ambayo awali matumizi ya vyoo hayakuwa na kipaumbele sana hivyo tunawakaribisha ili tuendelee kusaidiana kuwahudumia wanajamii wa Wilaya yetu."
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mikakati ya SAFE kwaajili ya kupunguza maambukizi ya Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemoTrakoma kwaniaba ya Dkt. George Kasibante Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Bi. Jubilate Temu amesema kuwa, kiwango cha maambukizi ya trakoma Wilayani Monduli kilikuwa asilimia 9.1 kwa mwaka 2022 ukilinganisha na asilimia 57.6 kwa mwaka 2006 kabla ya mikakati msonge mwaka 2015.
Aidha, Bi Jubilate amesema kupitia klabu hizo za SWASH mafunzo kwa Maafisa Afya, Waratibu wa SWASH na ANTDs yametolewa ili kuendelea kuelimisha Jamii kaya na mashule kuzingatia kanuni za usafi binafsi na wa Mazingira.
Bi. Jubilate ameeleza kuwa kupitia klabu za SWASH mashuleni yamekuwepo mafanikio makubwa ikiwemo Wanafunzi kupitia Elimu waliyoipata kwenye klabu, wameweza kuelimisha wazazi wao kwa kuwaeleza namna ugonjwa wa Trakoma unavyoambukiza, madhara yake na namna bora ya kujikinga na hivyo wazazi kuhamasika na kujenga vyoo na kuvitumia.
Kwa upande wake Bi. Noreen mmoja wa Bodi ya Wadhamini wa Helenkeller ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwaruhusu kufanya kazi kwa kushirikiana na wizara ya Afya ili kutokomeza ugonjwa wa Trakoma na kuboresha Afya za Watanzania.
Naye Nambris Logolye Mwanafunzi shule ya Msingi Orkeeswa, ameeleza mafanikio baada ya kupata Elimu ya trakoma kwamba familia yake imeweza kujenga choo na kuvitumia huku akieleza changamoto ya miundombinu ya maji kuwa kikwazo cha ufanisi shuleni hasa katika kuhudumia bustani ya maua na mbogamboga kwa bustani ya klabu yake ya SWASH shuleni.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli