Kamati za ujenzi ngazi za Shule kutoka katika kila shule iliyopatiwa mradi Wilayani Monduli leo Julai 16, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo zimepatiwa mafunzo ya namna bora ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa Miundombinu katika Shule tano (5) za Msingi ambazo ni Endepesi, Lemiyoni, Manyara Ranch, Loosimingori na Lowassa Wilayani humo.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo Ndg. Haruna Haji ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Happiness R. Laizer amesema kuwa; Serikali imetupatia jumla ya Shilingi milioni 669.1 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 18 na matundu 55 ya vyoo katika Shule hizo, ambapo fedha hizo zinapaswa kutumika kwa kuzingatia ubora, taratibu na miongozo ya Serikali.
Aidha, Ndg. Haruna amesisitiza kuwa wakati wa kutekeleza miradi hiyo wanakamati hao katika kila shule husika wahakikishe kusudio la Serikali linafikiwa na kwamba wakati wa utekelezaji wasiweke maslahi yao mbele bali maslahi ya Wananchi na Serikali kwa ujumla.
Naye Ndg. Lucas Haga ambaye ni Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu Wilayani humo amefafanua kuwa fedha hizo japo zimefika sasa itambulike kuwa ni za mwaka wa fedha 2024/2025 ambapo utekelezaji wake unafanyika katika mwaka 2025/2026, amesisitiza Kamati hizo kuzingatia majukumu yake ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.
Kwa upande wake Ndg. Elias Mollel mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ameshukuru kwa Elimu na maelekezo yaliyotolewa na kusema anaamini utekelezaji utaenda sawa sawa na maelekezo ili miradi ikamilike kwa wakati na kwa ubora.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli