Viongozi wa kimila ni nguzo muhimu katika jamii na mnapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa migogoro badala ya kuwa chanzo cha migogoro, ili kudumisha amani na kuleta Maendeleo endelevu katika Jamii.
Hayo yamesemwa leo Julai 24, 2025 na Bi. Gloriana Julius Kimath Mkuu wa Wilaya ya Monduli katika kikao chake cha kwanza na Malaigwanani (wazee wa Mila) hao Wilayani humo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo chenye lengo la kuwataka viongozi hao wa kimila kudumisha ushirikiano hasa katika masuala ya kutatua migogoro mbalimbali baina ya Wananchi na kuhakikisha Usalama unazidi kuimalika ndani ya Jamii.
Aidha, Bi. Gloriana Kimath amewataka Malaigwanani hao kuwa na mshikamano na wanajamii katika kuhakikisha wanasimamia vema masuala yenye kuleta tija kwa Jamii kwa kuwa wao ni chachu kubwa ya Maendeleo katika maeneo yao.
Naye Ndg. Isack Olekisongo ambaye ni Kiongozi wa Malaigwanani, ameshauri kuwa ni vyema panapotokea migogoro kabla ya kutolewa maamuzi ya migogoro hiyo kwakuwa ina mguso kwa wananchi, ni vyema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ishirikiane na malaigwanani ili kupata suluhu ya pamoja ambayo itasaidia kuondoka kabisa migogoro husika.
Kwa upande wake Ndg. Sekera Lemara, ambaye ni Laigwanani na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa, alitoa pongezi kwa uongozi wa Wilaya kwa kuitisha kikao hicho akieleza kuwa kikao hicho kimeongeza ari ya kutambulika kwa Malaigwanani hao na kwamba watahakikisha wanaendelea kulinda amani katika jamii
Mhe. Gloriana amehitimisha kikao hicho kwa kuwapongeza malaigwanani kwa kujitokeza kwa wingi na kwa ushiriki wao mzuri huku akiwasisitiza kuendelea kutoa hamasa kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2025
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli