Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Gloriana Julius Kimath mapema leo Julai 30, 2025, amefanya kikao kazi na Wakuu wa Divisheni na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya hiyo katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri kwa lengo la kuwakumbusha wajibu wao katika utendaji kazi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Gloriana amewataka Wakuu wa Divisheni na Vitengo Wilayani humo kuendelea kufanya kazi kwa moyo, weledi na Upendo, kwa kujitolea bila kutegemea malipo ya ziada, kushirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu ya Halmashauri, na kuhakikisha wanakuwa watumishi wa wananchi badala ya kujitenga, na kujiinua kwa watu wanaowatumikia
Aidha, Mhe. Gloriana amewaasa kuzingatia umuhimu wa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo, kulinda mali za umma kama magari na majengo, pamoja na kutumia lugha yenye staha katika utoaji huduma kwa jamii.
Naye Bi. Happiness R. Laizer Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo Bi. Gloriana Kimath kwa kusudio la kikao hicho na kusema kuwa kitasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji kazi na kuendelea kuleta Maendeleo endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Monduli huku akiahidi kuendeleza ushirikiano kati ya Ofisi yake na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo katika kuleta maendeleo wilayani humo.
Bi. Pamela Ijumba Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi amemshukuru Mhe. Gloriana Kimath kwa kuwakumbusha majukumu yao ya kiutumishi na maisha binafsi na kuahidi kushirikiana katika utendaji kazi kwa Maendeleo ya Halmashauri na wananchi kwa ujumla.
Sambamba naye,Huruma Mgeyekwa Kaimu Mkuu Kitengo cha ukaguzi wa ndani amesema kuwa kikao hicho kimeendelea kuongeza chachu ya utendaji kazi katika majukumu yao ya kila siku na kwamba katika mwaka huu mpya wa fedha wanatarajia kuona mabadiliko makubwa sana katika utendaji kazi
Mhe. Gloriana amehitimisha kikao hicho kwa kuwapongeza Wakuu wa Idara na Vitengo kwa kushiriki vyema katika kikao hicho huku akiwataka kuwa sehemu ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki vyema katika uchaguzi Mkuu Octoba 2025.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli