Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko amewataka wananchi Wilayani Monduli kutogawanyika kwa itikadi ya dini wala siasa hasa wakati huu tunapoelekea kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani kwa manufaa ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Aprili 23, 2025 wilayani humo wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Kata ya Esilalei mara baada ya kuzindua mradi wa maji katika Kijiji hicho na baadae katika eneo la Shule Mpya ya Sekondari ya Migungani One.
" Ninatamani kuona hatugawanyiki wala hatuwekwi kwenye makundi ya dini na ukabila, niwaombe wananchi wa Monduli pendaneni na shirikianeni, uchaguzi utakapofika najuwa watakuja wengi bali ninyi chagueni kwa haki." amesema Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Aidha, Mhe. Dkt. Biteko amewataka wananchi wa Monduli kuutunza mradi wa maji wa Esilalei pamoja na mradi wa ujenzi wa shule ya Sekondari Migungani One na miundombinu yake ili uendelee kutumiwa na watu wengine pia wajao.
Amewaasa Wanafunzi waliopo katika shule hiyo kutumia wakati huu kusoma kwa bidii kwakuwa ndio urithi pekee mzazi anaweza kutoa kwa mwanae kwa faida ya baadae.
Naye Mhe. Festo Kiswaga Mkuu wa Wilaya hiyo amesema kuwa Monduli ni Wilaya pekee ambayo shule zake zote za Sekondari ni za bweni hivyo ameahidi atahakikisha utunzaji wa Majengo hayo unakuwa mzuri.
Kwa upande wake Mhe. Fredy Lowassa Mbunge wa Jimbo hilo la Monduli amemuomba Mhe. Biteko kusaidia uwepo wa uzio katika shule hiyo ambapo Mhe. Dkt. Biteko ameelekeza mara baada ya kuanza kwa zoezi hilo msaada ukihitajika Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo awasiliane na OR- TAMISEMI ili uzio huo ujengwe.
Mhe. Dkt. Biteko amehitimisha kwa kuwapongeza Wizara ya Maji na RUWASA kwa kusimamia mradi huo vizuri na Pongezi nyingine kwa Menejimenti ya Monduli kwa kusimamia vizuri ujenzi wa shule ya Sekondari ya Migungani One.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli