Viongozi wa kata na vijiji wameagizwa kuhakikisha wanahamasisha,wanakusanya na kusimamia fedha za wananchi wanazozichanga ili zitumike kuboresha miundombinu za shule za sekondari katika wilaya ya monduli.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wiliya ya monduli Mh. Frank Mwaisumbe akifungua kikao kazi kilicho wakutanisha viongozi mbali mbali wa halmashauri ya wilaya ya monduli kilichofanyika leo 05/10/2021 chenye lengo la kujadili na kuweka mikakati ya ukusanyaji wa michango ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu sekondari.
Amesema Monduli ni miongoni mwa wiliya zenye changamoto ya miundo mbinu ya elimu nchini kutokana na monduli kuwa wilaya ya kwanza kuundwa Afrika Mashariki na kati na hivyo baadhi ya Miundo mbinu imechakaa kutokana na kujengwa muda mrefu.
Mwaisumbe amewaagiza viongozi hao kuwa wanapo kusanya fedha hizo ni lazima kila kiongozi akatoe mchanganuo wa matumizi ya fedha hizo kwa wanachi na kuhakikisha wanajibu maswali ya wananchi wanapo hoji juu ya michango hiyo.
Hata hivyo amesema kuna haja kutengeneza karakana ya halmashauri itakayo tumika kutengeneza madawati pamoja na vitanda ili kupunguza gharama zinazo tumika kutengeneza miundombinu hizo na kurahisisha upatikanaji wake kwa wakati.
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli Mhe. Isack Copriano ambaye amekiongoza kikao Kazi hicho amesema ili kufikia malengo waliyojiwekea na waliyo wekewa na serikali ni lazima kila mwananachi mwenye sifa atoe mchango huo kwa wakati na kusisitiza kuwa michango hiyo ni lazima kwa kila mmoja na siyo hiyari.
Amesema michango hiyo siyo kwajili ya kunufaisha wafanyakazi wa serikali bali ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Rais Samia Suluhu na pia ni kuhakikisha kizazi cha wilaya ya monduli kinapata elimu katika mazingira bora na salama.
Aidha ameunda timu maalum itakayo pitia katika kila kata wilayani monduli na ambayo itakuwa na jukumu maalumu la kuhamasisha na kutoa ufafanuzi juu ya michango hiyo na timu hiyo itaanza kazi katika kata ya engaruka.
Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya monduli Mhe. Raphael Siumbu amewaagiza viongozi wa kata kufanya kazi kwa kuzingatia mpango kazi na kila mmoja afanye majukumu yake kwa kufuata sheria kanuni na taratibu na kuzingatia ushirikiano ili kufikia malengo ya pamoja.
Katika hatua nyingine ametoa zawadi kwa kuwapongeza baadhi ya watendaji walio fanya vizuri katika ukusanyaji wa michango hiyo ya ujenzi wa miundo mbinu ya shule na kuwaagiza wengine kuwatumia kama mfano.
Kikao hicho kimeudhuriwa na viongozi mbali mbali wakiwemo Maafisa tarafa, madiwani,watendaji wa kata na vijiji pamoja na wenyeviti wa vijiji ambao mpaka kikao kinafungwa viongozi hao wamesema wamepokea na kukubali maagizo hayo na kuahidi kuwa watayatekeleza kama walivyo agizwa na kwa wakati ambapo siku ya mwisho ya kutoa mchango huo imependekezwa kuwa tarehe 30.11.2021
Imeandikwa na Kuchapishwa na
Obed Emmanuel
Ofisi ya TEHAMA Halmashauri ya Monduli
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli