Piki piki hizi tatu ninazowakabidhi Leo zitumike kwa kufanya majukumu mahususi yaliyokusudiwa na Serikali, ambayo ni kusimamia shughuli za usafi wa Mazingira katika Wilaya ya Monduli na si kwa matumizi binafsi Wala kwa matumizi ya biashara.
Hayo yamesemwa leo Novemba 22, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Monduli Mhe. Festo S. Kiswaga alipokuwa akikabidhi Piki piki hizo kwa Maafisa Afya wa Kata za Makuyuni, Lolkisale na Mto wa Mbu katika eneo la uwanja wa Halmashauri hiyo.
Katika tukio hilo, DC Kiswaga amesema " Maeneo ya pembezoni mwa barabara na maeneo ya magulio Kuna uchafu ama takataka nyingi ambazo si sawa kuwa katika maeneo hayo ambako zimetupwa ovyo kwa hiyo sasa kwakuwa tumepatiwa pikipiki hizi kwa ajili ya kusimamia shughuli za usafi hakikisheni kila eneo linafikiwa na kukaguliwa katika Kata zenu ili kuboresha usafi wa Mazingira katika maeneo yote.
Sambamba na hilo DC Kiswaga amesema kuwa uchafu ni chanzo cha mlipuko wa magonjwa hivyo tukiimarisha usafi katika Mazingira yetu tutakuwa tumeepuka magonjwa hayo. Hivyo kila mtu awe Kiranja wa mwenzake katika kuhakikisha hatutupi taka ovyo katika maeneo ya majumbani, kazini na katika maeneo ya biashara.
Akisoma taarifa ya usafi wa Mazingira wakati wa kukabidhi pikipiki hizo Bi. Happiness R. Laizer Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli amesema " Idara ya Afya kupitia sehemu ya afya Kinga imepewa jukumu la kuhakikisha wananchi wanaishi katika Mazingira bora safi na salama yanachochea afya na ustawi wa jamii.
Naye Ndg. Isaack Copriano Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli ametoa shukrani kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pikipiki hizo huku akiwakumbusha watumishi wote kujitokeza kushiriki Uchaguzi ifikapo Novemba 27, 2024.
.Kwa upande wake Bi. Haika Benard Temba Afisa Afya Kata ya Mto wa Mbu kwa niaba ya wenzake waliokabidhiwa pikipiki hizo amesema kuwa kupata piki piki hizo kutaboresha zaidi utendaji kazi wao kwa kuwa watakuwa wanakagua maeneo mengi kwa muda mfupi ikiwemo katika maeneo ya zahanati, masoko na minada na kuhakikisha usafi umeimarika.
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli