Taka siyo uchafu bali ni raslimali ambayo ikisimamiwa vizuri inaweza kubadilika na kuwa bidhaa zenye thamani kama mbolea, nishati, au malighafi kwa Viwanda ili kuzalisha bidhaa nyingine muhimu kwa matumizi ya Jamii.
Hayo yamesemwa leo Septemba 20, 2025 katika viwanja vya soko la Makuyuni na Ndg. Kelvin Evod Mmanda ambaye ni Afisa Tarafa wa Tarafa ya Makuyuni kwa niaba ya Mhe. Gloriana Kimath Mkuu wa Wilaya ya Monduli; alipokuwa akizungumza na Wananchi katika Maadhimisho ya siku ya usafishaji Duniani ambayo hufanyika kila mwaka na zaidi ya nchi 191 Duniani.
Ndg. Kelvin Evod Mmanda amesema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuishirikisha Jamii, Taasisi na Sekta binafsi katika zoezi la kupambana na changamoto ya taka mbalimbali katika maeneo tunayoishi, maeneo ya Biashara, maeneo ya kazi na maeneo ya masoko na kuwa na suluhisho la pamoja ili kuyaweka Mazingira katika hali ya usafi lakini pia kuwa na Jamii yenye Afya njema.

Naye Ndg. Fredrick Mnahela Afisa Mazingira katika Wilaya hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo amesema kuwa Usafi si tu jukumu letu bali ni Uwekezaji katika Afya, uchumi na Mazingira endelevu. Katika maadhimisho haya ya siku ya usafishaji Duniani, tukumbuke kuwa kila taka ina thamani kama tutaiona kwa jicho la sahihi.
Aidha, Ndg. Fredrick Mnahela ameeleza kuwa taka za plastiki zaweza kuzalisha vigae, au vifaa vya matumizi ya nyumbani, mabaki ya chakula yaweza kuwa mbolea huku taka ngumu zikizalisha nishati mbadala na kupunguza utegemezi wa Kuni na mkaa.
Kwa upande wake Bi. Rahma Mkazi wa Makuyuni amesema kuwa suala la usafi ni muhimu kwa Jamii huku akitoa hamasa Wananchi wenzake kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi kuanzia ngazi ya Kaya ili kuweka Mazingira katika hali ya usafi.

Ndg. Kelvin Mmanda amewasisitiza wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi kila siku na kushiriki zoezi hilo siku za jumamosi ya mwisho wa mwezi, kutotupa taka hovyo, na kuzingatia suala la ujenzi wa vyoo bora na kuvitumia kwa usafi ili kulinda Afya zao.

Kaulimbiu: " Tunza Mazingira kwa kuzipa taka thamani. "
Monduli District Council
Sanduku la Posta: P.O BOX 1 Monduli
Namba ya simu: +255 - 27- 2538006
simu ya mkononi:
Barua Pepe: ded@mondulidc.go.tz
Hatimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Monduli